Na; Lunanilo Ngela
Mkuu mpya wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Dkt. Stephen Isaac Mwakajumilo mapema Oktoba 18, 2023 amekutana na wafanyabiashara wa mji wa Mangaka na Kilimanihewa ili kujitambulisha, kupokea na kutatua kero za wafanyabiashara hao ikiwa ni pamoja na kuelezea mipango na mikakati atakayoanza nayo katika kipindi cha uongozi wake.
Akizungumzia suala ya ujenzi wa mji wa Mangaka na Kilimanihewa Dkt. Mwakajumilo amewaeleza wajumbe kuwa, Wilaya inaratibu mpango wa ujenzi utakaoboresha muonekano wa uso wa mji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha ujenzi wa maghorofa, uwekaji wa taa za barabarani pamoja na kutenga maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati, Viwanda na Mahoteli.
“Miaka miwili ijayo Nanyumbu haitakuwa hivi,” alisema Dkt. Mwakajumilo akielezea namna mpango wa uhamasishaji wa ujenzi wa mji mpya utakavyokuwa na matokeo chanya huku Serikali ikijikita katika kutekeleza ujenzi wa miundombinu mhimu ikiwemo ujenzi wa soko la Wilaya ya Nanyumbu.
Katika mwaka wa Fedha 2023/2024 Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa katika miji ya Mangaka na Kilimanihewa, ikiwemo Ujenzi wa Shule Mpya ya Awali na Msingi Kilimanihewa unaogharimu Shilingi Milioni 608.2 na Ujenzi wa Shule mpya ya Kitaifa ya Wasichana Naishero unaogharimu shilingi Bilioni 3.
Miradi mingine ni Ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha Lami ikiwemo barabara ya Likungwa na Msangi yenye urefu wa Kilomita 1.2 unaogharimu Shilingi Milioni 948.5, Mradi wa Maji toka Mto Ruvuma unaogharimu Shilingi Bilioni 38.1 na Mradi wa Maji Sengenya wenye thamani ya shilingi Bilioni 3.6.
Hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu imeonekana kuwavutia wafanyabiashara waliohudhuria kikao hicho kutoka makundi mbalimbali wakiwemo Maafisa Usafirishaji (boda boda) na mama lishe, ambao muda wote wa kikao walikuwa wakipiga makofi na kumshangilia Mhe. Mwakajumilo.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.