Mkuu wa Wilaya ya Nayumbu Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo akizungumza katika mkutano wa wadau wa maji Nanyumbu
Na, Lunanilo Ngela
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji, imeipatia Wilaya ya Nanyumbu Shilingi 5,376,841,442.54 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji kwa mwaka wa Fedha 2022/2023.
Haya yamebainishwa katika mkutano wa wadau wa maji uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mapema leo Mei 30, 2023 ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Chaurembo na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, madiwani wa Halmashauri, vyama vya siasa, watumishi wa Umma, pamoja na jamii za watuma maji.
Mheshimiwa Chaurembo amempongeza Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Simoni Mchucha, pamoja na watendaji wa Idara hiyo kwa kusimamia kikamilifu na kutekelezaji miradi mbalimbali ya maji kwa vijiji 59 kati ya 89 vinavyohudumiwa na RUWASA wilayani hapo. Aidha, amezitaka jumuiya za watumia maji kuhakikisha miradi hiyo ya maji inajiendesha, ikiwa ni pamoja na kusoma mapato na matumizi ya miradi kwa wananchi.
Naye Kaimu Meneja wa RUWASA Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha, amewaeleza wajumbe kuwa, Bilioni 5.3 zilizotolewa na Serikali zinatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa maji Kamundi, Likokona II, Mitumbati – Chilunda pamoja na upanuzi na ukarabati wa bwawa la maji Sengenya. Aidha, utafiti wa maji na uchimbaji wa visima sita unafanyika vijiji vya Mkwajuni, Chihuve, Rukumbi, Lumesule, Mpombe na Mbangala Mbuyuni.
Mhandisi Mchucha ameongeza kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 shilingi 2,086,419,158.00 zitatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maji ikiwemo; Ujenzi wa Mradi wa Maji Mburusa na Michiga, ukarabati wa mradi wa maji Ndwika, Holola na Chivilikiti, uboreshaji wa mradi wa maji Mtawatawa na Nakopi.
Aidha, katika bajeti hiyo ya 2023/2024 visima kumi vitachimbwa kwa ajili ya utafutaji wa vyanzo vya maji katika vijiji vya Mtalikachau, Chipuputa, Lukwika, Mnanje A, Marumba, Namarupi, Mchenjeuka, Namaka, Nanderu na Nahawara.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Nanyumbu Cde. Rashid Mrope amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyopeleka fedha nyingi wilayani hapo kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo.
Serikali ya awamu ya sita imeshaanza utekelezaji wa mradi kubwa wa kimkakati wa maji toka mto Ruvuma Kwenda Mangaka unaogharimu shilingi Bilioni 38.7 kupitia mkandarasi M/S AFCONS INFRASTRUCTURE LTD pamoja na Mtaalam Mshauri WAPCOS LTD.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.