Katika picha ni Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza na wanachi wa kijiji cha Mitumbati wilayani Nanyumbu
Na, Lunanilo Ngela
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed amezindua mradi wa maji wa Mitumbati-Chilunda wilayani Nanyumbu wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.35 zilizotokana na Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19 pamoja na Programu ya PforR unaolenga kutatua kabisa tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika vijiji vya Mitumbati na Chilunda.
Akizindua mradi huo katika maadhimisho ya Wiki ya Maji ambayo kimkoa imefanyika wilayani Nanyumbu, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa mradi wa Mitumbati-Chilunda ni moja kati ya miradi mingi ya maji iliyotekelezwa mkoani Mtwara katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan. Aidha, Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi kutunza miundombinu ya maji kwa kushirikiana na mamlaka za maji, kutunza vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kuheshimu mipaka iliyowekwa ili kulinda vyanzo hivyo vya maji.
Katika maadhimisho hayo, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed aliambatana na wakuu wa Wilaya nne za Mkoa wa Mtwara akiwepo Mkuu wa Wilaya mwenyeji Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo, Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Lauter John Kanoni, Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mhe. Kanali Patrick Kenan Sawala pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Mwangi Rajabu Kundya.
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Chaurembo akizungumzia suala la upatikanaji wa maji wilayani Nanyumbu amesema kuwa, pamoja na Serikali kutekeleza Mradi wa Mitumbati-Chilunda pia Serikali inatarajia kutekeleza mradi mkubwa wa Maji kutoka mto Ruvuma wenye thamani ya shilingi Bilioni 40. Miradi mingine inayotekelezwa wilayani Nanyumbu ni pamoja na mradi wa ukarabati na utanuzi wa bwawa la Sengenya unaogharimu shilingi Bilioni 3.6, Ujenzi wa bwawa la Maratani wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.2 na uchimbaji wa visima 10 vyenye thamani ya shilingi milioni 480 ambao umeshakamilika.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji nchini hufanyika Machi 22 kila mwaka ikiwa ni utekelezaji wa Azimio Na. 47/193 la Umoja wa Mataifa (UN) linalolengo kuunganisha mataifa katika kutathimini utekelezaji, mafanikio na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maji. Aidha, azimio hili huyafanya mataifa kuainisha mikakati ya kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira na kusimamia utunzaji wa rasilimali ya maji.
Kauli Mbiu ya Wiki ya Maji kwa Mwaka 2023 ni “Kuongeza Kasi ya Mabadiliko katika Sekta ya Maji kwa Maendeleo Endelevu ya Kiuchumi”
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akikagua tanki la maji kwenye mradi wa Mitumbati-Chilunda
Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba Mhe. Kanali Patrick Sawala (wa kwanza kulia), Mhe. Mwangi Kundya Mkuu wa Wilaya ya Newala (wa pili kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Masasi Mhe. Lauter Kanoni (wa nne kutoka kulia) wakiwa katika mradi wa maji
Mkuu wa Mkoa akifungua jiwe la msingi kwenye mradi wa maji Mitumbati-Chilunda
Kaimu Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Simon S. Mchucha akielezea hatua mbalimbali za utekelezaji wa Mradi mbele ya Mkuu wa Mkoa (wa pili kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe Mariam Chaurembo (wa kwanza kushoto) na viongozi wengine walioshiriki maadhimisho hayo
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Nanyumbu Ndg. Ibrahim J. Mwanauta
Mkuu wa mkoa wa Mtwara (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mwekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mtwara (wa pili kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Benjamin Masimbo (wa kwanza kulia)
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.