Na, Lunanilo Ngela
Wajumbe wa Kamati ya Lishe Wilaya ya Nanyumbu wamekutana mapema Novemba 10, 2023 katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri kupokea na kujadili masuala mbalimbali yahusuyo afya.
Katika kikao hicho, wajumbe wamepokea taarifa ya utafiti uliofanywa na maafisa lishe Nanyumbu kuchunguza aina ya chumvi inayotumiwa na wanyeji na kubaini uwepo wa kaya zinazotumia chumvi isiyo na madini joto.
“Tulikwenda Shule za Sekondari Mangaka na Sengenya pamoja na Shule za Msingi Kilimanihewa na Mangaka tukawaagiza wanafunzi watuletee sampuli ya chumvi wanazotumia nyumbani ambapo jumla ya sampuli 620 kati ya 890 sawa na asilimia 69 pekee zilikuwa na madini joto,” alisema Francis Mmanda Afisa Lishe Wilaya.
Madini joto ni moja ya kirutubisho muhimu kwa ukuaji mzuri wa akili na mwili wa binadamu na endapo mtu atakuwa na upungufu wa madini joto basi anaweza kupata madhara mbalimbali ikiwa ni pamoja na udumavu wa akili na mwili.
Ripoti iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF likishirikiana na Shirika la GAIN (2018) inasema kuwa, “Takriban watoto milioni 19 ambao ni sawa na asilimia 14 ya watoto wanaozaliwa kila mwaka, wako hatarini kupata matatizo ya ubongo kutokana na uhaba wa madini joto mwilini mwao, madini ambayo yanapatikana kwenye chumvi.”
Nao wajumbe wa Kamati ya Lishe wamewataka wafanyabiashara kuhakikisha chumvi wanayoiuza kwa walaji inakuwa na madini joto ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaouza chumvi isiyokidhi viwango.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.