Na; Lunanilo Ngela
Wamakua (Makhua) ni kabila maarufu la kibantu linalopatikana maeneo ya Msumbuji, kwa kiasi kikubwa kaskazini mwa Mto Zambezi pamoja na Tanzania hususani Mikoa ya Mtwara na Lindi.
Kabila hili hujihusisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, uvuvi, ufugaji, uchongaji, ususi na sanaa ya nyimbo za jadi.
Ukiachana na shughuli zingine za kiuchumi zinazofanywa na wamakua wa maeneo mbalimbali ikiwemo Nanyumbu, leo tutajikita kwenye kilimo na hususani kilimo cha korosho.
Katika miaka ya 1960 mpaka 1985 huko Dar es Salaam Wilaya ya Ubungo kulikuwa na sehemu yenye mashamba makubwa ya mikorosho inayomilikiwa na wanakijiji mbalimbali wa kabila la Wamakua ikiwemo Wayao, Wangindo na Wamakonde.
Mashamba yale yalipata umarufu mkubwa kutoka na watu wengi kwenda kula matunda yanayoitwa “mabibo” kwenye mikorosho hiyo.
Wamiliki wa mashamba yale walikuwa wakarimu sana ambao waliruhusu watu kula mabibo ingawa waligeuka mbogo ikiwa mtu atatoka na korosho badala ya mabibo kwenye mashamba yao, yaani siku hiyo “angekiona cha mtema kuni.”
Makundi makubwa ya watoto kutoka maeneo mbalimbali wakati wakiwinda kitoweo hususani sungura, waliingia katika mashamba hayo kula mabibo na kufanya eneo hilo kuwa maarufu sana na kupewa jina la “Mabibo.”
Ukiwa Dar es Salaam Wilaya la Ubungo utakutana na Kata ya Mabibo yenye mitaa sita ikiwemo Matokeo, Mabibo, Farasi, Azimio na Kanuni ambayo asili ya maeneo hayo ni mashamba yaliyokuwa na matunda maarufu kwa jina la “Mabibo.”
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.