Na; Lunanilo Ngela
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mapema leo Septemba 17, 2023 amefanya ziara ya kikazi Wilaya ya Nanyumbu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.
Katika ziara hiyo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua ghala na miundombinu ya Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu (TANIPAC) wenye thamani ya shilingi Bilioni 1.1 katika eneo la Naishero Kata ya Mangaka.
Rais Samia amezungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kumpokea mjini Mangaka ikiwa ni pamoja na kupokea na kutatua kero za wananchi hao zilizowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Yahya Ally Mhata.
Naye Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Salvio Kapinga akitoa majibu ya utatuzi wa kero ya kukatika katika kwa umeme Nanyumbu amewaeleza wananchi kuwa, Rais Samia ametoa fedha za kutekeleza mradi wa Gridi Imara Songea - Masasi huku awamu ya pili (phase II) inayogharimu Bilioni 200 ikihusisha ujenzi wa njia (line) na vituo vya kupoozea umeme Tunduru – Masasi mradi ambao tayari umeshaanza.
Rais Samia ameipatia Wilaya ya Nanyumbu gari tatu za kubebea wagonjwa (ambulance) ili kuboresha upatikaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia wananchi hao juu ya uhakika wa soko la mazao ikiwemo mbaazi na ufuta.
Wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu kupitia Mbunge wa Jimbo Mhe. Yahya Ally Mhata wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa dhamira yake ya dhati inayolenga kumaliza kabisa kero ya uhaba wa maji Nanyumbu kwa kutoa mabilioni ya fedha ikiwemo Bilioni 38 za mradi wa maji Ruvuma, Bilioni 3.6 Mradi wa Maji Sengenya na Bilioni 3.2 mradi wa maji Maratani.
Aidha, wananchi hao wametoa shukrani kwa fedha za miradi mingine ya maendeleo ikiwemo Elimu, Afya, Miundombinu ya Umeme na Barabara zilizotolewa na Rais Samia kwa awamu tofauti tofauti ili kuboresha huduma za jamii.
Rais Samia leo Septemba 17, 2023 anahitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Mtwara iliyoanza Septemba 14, 2023.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.