Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nayumbu Ndg. Ibrahim John Mwanauta (kushoto) akifyeka nyasi katika eneo la hospitali ya wilaya
Na, Lunanilo Ngela
Katika kuadhimisha siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao huadhimishwa Aprili 26 ya kila mwaka, watumishi wa umma na wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu wameungana kwa pamoja na kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya hospitali ya Wilaya iliyopo mjini Mangaka.
Viongozi mbalimbali wa Wilaya akiwepo Ndg. Baraka Mlahagwa aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Ibrahim Mwanauta na Katibu wa Chama Cha Mapinduzi wa Wilaya Bi. Salome Luhingulanya wakizungumza na wananchi waliojitokeza kufanya usafi hospitalini hapo, wameyaelezea matunda ya muungano ikiwemo tunu ya amani na utulivu nchini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kiwilaya iliyofanyika Machi 6, 2023 kijiji cha Mchenjeuka Bi. Martha Nanyaka amekabidhi kitanda maalumu kwa ajili ya zoezi la kuchangia damu (blood donating bed) chenye thamani ya shilingi milioni moja na elfu arobaini na tano zilizochangwa na wanawake ikiwa ni sehemu ya mchango wao kwa hospitali hiyo katika maadhimisho ya siku ya Muungano.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliundwa Aprili 26, 1964 ikiwa ni Muungano wa Mataifa mawili huru ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambayo yaliingia mkataba wa Muungano mnamo mwaka 1964 na kuanzishwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkataba wa Muungano ulitiwa saini na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Aprili 22, 1964 huko Zanzibar.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.