Katika picha ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri nane wa Kisekta Mhe. Dr. Angeline Sylvester Mabula (katikati) akiwasili katika kijiji cha Wanika
Na, Lunanilo Ngela
Serikali kupitia Kamati ya Mawaziri nane wa Kisekta ikiongozwa na Mhe. Dr. Angeline Mabula (Mb) ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, imekutana na wananchi wa vitongoji vya Livambangoma, Wanika, Namaromba na Nambunda wilayani Nanyumbu wanaoishi kwenye hifadhi ya msitu Mbangara na kuwatengenezea mpango wa makazi mapya wananchi hao ili kupisha eneo la hifadhi.
Akizungumza na wananchi hao Mhe. Dr. Mabula amesema kuwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ikishirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu itaandaa utaratibu mzuri wa kuwagawia maeneo wananchi hao katika vijiji mama yaani Mbangara Mbuyuni na Marumba. Aidha, ameongeza kuwa serikali itahakikisha zoezi hilo linafanyika kwa utulivu na kila mwananchi anatendewa haki.
Katika ziara hiyo Mhe. Mabula aliongozana na Mhe. Balozi, Dr. Pindi Chana (Mb) Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Maryprisca Mahundi (Mb) Naibu Waziri wa Maji na Mhe. Khamis Hamza Khamis (Mb) Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali. Ahmed Abbas Ahmed akizungumza na wanachi hao amesema kuwa Serikali ina mpango mzuri wa matumizi ya ardhi na hivyo kuwataka wananchi kuwa watulivu wakati serikali ikiwaandalia wananchi hao uratatibu wa makazi. Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Marium Chaurembo ameishukuru Serikali chini ya Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuipatia Nanyumbu Miradi ya maendeleo ikiwemo Mradi wa maji wa mto Ruvuma. Aidha, mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Yahya Ally Mhata ameiomba Serikali kuendelea kushirikiana na wananchi wa vijiji hivyo kwani wana mchango mkubwa katika shughuli za maendeleo nchini.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.