Katika picha ni Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo akizungumza na wajumbe wa Kikao cha tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023
Na, Lunanilo Ngela
Rais wa Jamhui ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan ameipatia Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Shilingi 1,687,350,000.00 ikiwa ni kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari kwa mwaka 2022/2023.
Akizungumza katika kikao cha tathmini ya Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo amesema kuwa, Rais Samia ameendelea kuing’arisha sekta ya Elimu Nanyumbu kwa kuiingizia fedha nyingi za miradi ya ujenzi ikiwemo fedha hizo.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ametoa onyo kali kwa watendaji wote wa serikali, Kamati za Ujenzi pamoja na mafundi watakaobainika kuihujumu miradi hiyo kwa namna yeyote na kwamba hatasita kuwachukuliwa hatua kali za kisheria.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Ndg. Ibrahim John Mwanauta akitoa taarifa ya ujio wa fedha hizo ambapo shilingi 598,250,000.00 zinatoka Serikali Kuu na shilingi 1,089,100,000.00 zikitoka Mradi wa BOOST alisema kuwa, Fedha hizo za Mpango na Bajeti ya Maendeleo kwa mwaka 2022/2023 zitatekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji wa hosteli 3 kwa Shule za Sekondari Nanyumbu, Masuguru na Nangomba.
Miradi mingine ni Ukarabati wa Miundombinu ya Shule za Msingi Lukula na Nauru, Ujenzi wa nyumba za walimu Shule za Msingi Chungu, Liunga, Mitumbati na Mbangarambuyuni, Ujenzi wa matundu ya vyoo Shule Shikizi za Igunga/Masiyalele na Kisimatuli/Magomeni. Fedha hizo pia zitatumika kukamilisha ujenzi wa maboma ya madarasa kwa Shule nne za Msingi ikiwemo Mpombe, Mbangarambuyuni, Chigweje na Lumesule.
Aidha, Fedha za Mradi wa BOOST zimeelekezwa kwa Shule za Msingi Kilimanihewa, Namaka, Lumesule, Msinyasi, Kazamoyo na Chihuve alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.
Nao waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu ambao pia ni wawakilishi wa wananchi katika Kata wanazoziongoza, wamemshukuru sana Mhe. Rais Samia kwa namna anavyopeleka fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali wilayani humo ikiwemo miradi ya Elimu. Aidha, waheshimiwa madiwani hao wameahidi kuisimamia Halmashauri kikamilifu katika kutekeleza miradi yote iliyoingiziwa fedha.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.