Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu
Na, Lunanilo L. Ngela
Katika mkutano uliofanyika viwanja vya mabasi Mjini Mangaka, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amewaeleza wananchi wa Nanyumbu juu ya Mradi mkubwa wa maji wa mto Ruvuma uliotengewa zaidi ya shilingi Bilioni 80 ili kusambaza maji wilayani humo.
Mradi huo ambao ni utekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi unatarajia kuanza mapema mwezi Novemba na tayari mkandarasi amekwishapatikana na usanifu wa mradi umekamilika.
Waziri Mkuu amesema nia ya Serikali ni kumtua mwanamke ndoo. Aidha, ameongeza kuwa kampeni ya kumtua mwanamke ndoo haitaishia vijijini na mijini tuu bali sasa inakwenda mpaka ngazi ya vitongoji na visiwa.
Akizungumzia suala la miundombinu ya usafiri Mhe. Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha 2020-2025 Serikali itajenga reli ya kisasa toka Mtwara mpaka Mbamba Bay Ruvuma ikipitia wilayani Nanyumbu. Aidha, Barabara ya Nanyumbu - Nachingwea mpaka Morogoro pamoja na barabara za lami mjini Mangaka zitajengwa katika kipindi hicho ili kuendelea kurahisisha huduma za usafiri.
Waziri Mkuu akizungumzia suala ka korosho amesema Serikali itaendelea kuhakikisha wakulima wanauza korosho zao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ili kumsaidia mkulima kupata bei nzuri na kutodhurumiwa na wafanyabiashara. Aidha, ametoa maelekezo kuwa mkulima au mfanyabiashara asikatwe unyaufu kwani korosho inanyauka baada ya miezi sita.
Akizunguzia suala la Elimu amesema katika kipindi cha 2020-2025 Serikali itajenga mabweni kwa shule zote za sekondari za Serikali ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira tulivu.
Ndugu Majaliwa Kassim Majaliwa (MNEC) ameomba kura za ndiyo kwa mgombea wa kiti cha urais Ndg. John Pombe Magufuli kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi pamoja na wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho. Aidha, Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Tarehe 28/10/2020 nchini pote na hivyo amewakumbusha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.