Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Yustus Mmuni akizungumza na Walimu katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mangaka
Na, Lunanilo Ngela
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri na Mjumbe wa Kamati za Fedha, Utawala na Mipango pamoja na Kamati Shirikishi ya Kudhibiti UKIMWI Mhe. Yustus Mmuni, ametowa motisha kwa walimu na wanafunzi wa Shule za Awali, Msingi na Sekondari zenye thamani ya shilingi milioni 18.2 kutoka Mfuko wa Motisha za Elimu.
Mhe. Mmuni akitoa motisha hizo kwa walengwa mapema leo Juni 05, 2023 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mangaka amesema kuwa, nia ya Mkuu wa Wilaya na wadau wa Elimu ni kuona Wilaya inafanya vizuri kitaaluma kwa Shule za Awali, Msingi na Sekondari.
Walimu waliofaulisha vizuri katika mitihani ya Shule za Msingi na Sekondari pamoja na waliowezesha wanafunzi wa darasa la pili kumudu stadi za KKK (Kusoma Kuandika na Kuhesabu) na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani ya Taifa wamepewa zawadi ya fedha. Aidha, vitabu vyenye thamani ya shilingi1,160,000 vimetolewa kwa shule za sekondari ili kurahisisha zoezi la ufundishaji na ujifunzaji shuleni.
“Mfuko wa Motisha za Elimu Nanyumbu” ni mfuko ulianzishwa na Mkuu wa Wilaya Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo na kuungwa mkono na wadau mbalimbali wa Elimu kwa lengo la kuinua kiwango cha Elimu kwa Shule za Awali, Msingi na Sekondari.
Katika harakati hizo za kuinua kiwango cha Elimu, Nayumbu imefanikiwa kufaulisha wanafunzi wote waliofanya Mtihani wa Kidato cha Sita Mwaka 2022 wilayani hapo kwa kupata daraja la kwanza mpaka la tatu pekee. Jumla ya watahiniwa 20 kati 59 walipata daraja la kwanza, 35 daraja la pili na wanne waliobaki wakipata daraja la tatu. Aidha, Shule ya Sekondari Chipuputa ilifanikiwa kufuta kabisa daraja ziro katika matokeo ya mitihani ya kidato cha nne 2022.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.