Kanali Ahamed Abbas Ahmed Mkuu wa Mkoa wa Mtwara akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mikuva
Na, Lunanilo Ngela
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Ahamed Abbas Ahmed amekutana na wananchi wa Kijiji cha Mikuva mapema leo Septemba 19, 2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika zahanati ya Mikuva ili kusikiliza na kupokea kero na changamoto zinazowakabili wananchi hao.
Mkutano huo ni utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipotembelea Wilaya ya Nanyumbu Septemba 17, 2023 na kuletewa ombi la wananchi hao lililowasilishwa na Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Mhe. Yahya Ally Mhata juu ya ahadi ya ujenzi wa Kituo cha Afya inadaiwa kutolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi mwaka 1988, wakati Kijiji hicho kikiwa ndani ya Wilaya ya Masasi.
Ahadi hiyo inadaiwa kutolewa takribani miaka 17 kabla ya Wilaya ya Nanyumbu kuanzishwa na kutangazwa rasmi kuwa Wilaya Julai 29, 2005 na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa na baadae Halmashauri kuanzishwa na kutangazwa Julai 01, 2007 katika Gazeti la Serikali Na. 190.
Wananchi hao wa Kijiji cha Mikuva kilichopo Kata ya Mnanje ambayo ina Kituo kingine cha Afya takribani Kilomita 6 kutoka kijijini kwao, wamemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa kiu yao ni Kutapa Kituo cha Afya.
Katika mkutano huo Mkuu wa Mkoa aliambatana na watendaji mbalimbali wa Serikali na Chama ngazi ya Mkoa na Wilaya akiwepo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara Ndg. Said Nyengedi ambaye amewaeleza wananchi hao namna Rais Samia anavyopambana kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.
Wananchi wa Kijiji cha Mikuva wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu na watendaji wa Chama na Serikali kwa kufanikisha Mkutano huo. Aidha, wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa nafasi wananchi hao ya kutoa Mawazo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mikuva
Katika picha ni baadhi ya wananchi wakiwasilisha changamoto zao kwa Mkuu wa Mkoa
Katika picha ni baadhi ya wananchi wakiwasilisha changamoto zao kwa Mkuu wa Mkoa
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.