Katika picha ni Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mtwara Ndg. Abuu Athuman Yusuph (katikati) akiwa na wajumbe wa UVCCM Mkoa walipotembelea Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu
Na, Lunanilo Ngela
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Mtwara Cde. Abuu Athuman Yusuph, ametoa pongezi za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Wilaya ya Nanyumbu fedha kwa awamu tofauti tofauti kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mwenyekiti huyo akiwa ameongozana na wajumbe wa UVCCM Mkoa wa Mtwara, ametoa pongezi hizo mapema leo Mei 15, 2023 alipotembelea miradi mbalimbali ya maendeleo Nanyumbu ikiwemo Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari Naishero iliyogharimu Shilingi Milioni 470 kutoka serikali kuu na Milioni 53 kutoka mapato ya ndani.
Miradi Mingine iliyotembelewa na Umoja wa Vijana ni pamoja na jengo la dharula la hospitali ya Mangaka lililogharimu shilingi milioni 353.5, barabara ya kiwango cha lami Mangaka – Nachingea border na Bomani yenye urefu wa kilomita 1.071 inayogharimu shilingi 719,398,973.75, ghala la kuhifadhia mazao Naishero lenye thamani ya shilingi Bilioni 1.128, ujenzi wa shule mpya ya msingi Kilimanihewa unaogharimu shilingi milioni 608.2 pamoja na kikundi cha Vijana (Development Group) kilichokopeshwa na Halmashauri shilingi milioni 20 kupitia mfuko wa Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu.
Katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa aliongozana na Cde. Julius John Simalenga Katibu wa UVCCM Mkoa, Cde. Rehema Ismail Ally ambaye ni Katibu Hamasa/Chipukizi Mkoa, Cde. Sameer Murji Mjumbe Baraza kuu UVCCM Taifa, Fahdin Chikopa Mwenyekiti wa Seneti Mkoa, Nasim Makombe katibu Seneti Mkoa pamoja na Shaibu Mohamed Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Mkoa.
Naye diwani wa Kata ya Mangaka Mhe. Halima Stamili Mchoma akizungumza katika shule ya sekondari Naishero, amewapongeza wajumbe wa umoja huo kwa kufanya ziara wilayani Nanyumbu kuona namna Ilani ya Uchaguzi 2020 ilivyotekelezwa katika kipindi cha Julai 2022 hadi Aprili 2023. Aidha, amewashukuru watendaji wa serikali na wananchi kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani hapo.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.