Viongozi wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali wilayani Nanyumbu wakiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Wilaya Mhe. Mariam Chaurembo (aliyekaa katikati)
Na, Lunanilo Ngela
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Mhe. Mariam Khatibu Chaurembo amewataka watendaji wa Halmashauri kutoa ushirikiano wa kitaalam katika uandishi wa maandiko ya miradi kwa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali yaliyopo wilayani Nanyumbu pindi unapohitajika ili kuyawezesha mashirika hayo kupata fedha za miradi yenye tija kwa maendeleo ya jamii.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa ushauri huo mapema leo Mei 25, 2023 katika Mkutano wa mwaka wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali Nanyumbu, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri na kuhudhuriwa na watumishi mbalimbali wa umma pamoja na viongozi wa mashirika saba yasiyokuwa ya kiserikali yaliyomo wilayani humo.
Viongozi wa mashirika hayo wamweleza Mkuu wa Wilaya kuwa, changamoto kubwa inayowakabili ni kukosekana kwa fedha za wafadhili huku baadhi ya maandiko yao ya miradi yakikosa vigezo, na hivyo Mkuu wa Wilaya kuwataka wataalam wa Halmashauri, kutoa ushirikiano wa kitaalam katika uandishi wa maandiko ya miradi kwa mashirika hayo yenye mchango mkubwa katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo katika nyanja mbalimbali ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Nanyumbu Ndg. Salum Abdul Palango pamoja na Mwakilishi wa Mkurugenzi ambaye pia ni Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Ndg. Philipo Sengela, wameahidi kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo ambayo yapo kisheria na kusimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002, iliyofanyiwa marekebisho na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Juni, 2005 kupitia Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali Na. 11 ya mwaka 2005, na Sheria Na. 3 ya mwaka 2019, inatoa tafsiri ya Shirika Lisilo la Kiserikali kuwa ni “Kikundi binafsi na cha hiari cha watu au mashirika, kisicho cha kisiasa wala kidini, kisicho cha kugawana faida, ambacho kimeundwa katika ngazi ya jamii kitaifa na kimataifa, chenye dhamira ya kukuza malengo halali ya kiuchumi, kijamii au kiutamaduni, kuhifadhi mazingira, kulinda na kutetea haki za binadamu na utawala bora katika jamii”.
Wilayani Nanyumbu Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali yamejipambanua kujikita katika masuala yahusuyo afya, elimu, Michezo, msaada wa kisheria, utetezi wa haki za watoto, pamoja na shughuli za kilimo. Aidha, utekelezaji wa miradi hiyo hutegemea zaidi fedha za wafadhili.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.