Mgombea Mwenza wa urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi Ndg. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu
Na, Lunanilo L. Ngela
Akiwa katika Mji wa Mangaka Ndg. Samia Suluhu Hassan, amewaeleza wananchi dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ya kumaliza kabisa kero ya maji wilayani Nanyumbu kupitia Mradi Mkubwa wa maji wa Mto Ruvuma. Usanifu wa Mradi huo umekamilika.
Pamoja na Mradi huo, Serikali katika kutekeleza ilani ya CCM ya 2015-2020 imetekeleza miradi mbalimbali ya maji wilayani Nanyumbu ukiwepo Mradi wa maji Nandete unaogharimu Shilingi milioni 285.499. Miradi ya maji ya lipa kulingana na matokeo (P4R) yenye thamani ya Bilioni 1.3 ipo hatua mbalimbali katika vijiji vya Nangomba/Mjimwema, Mkwajuni/Mikangaula na Kisimatuli/Masyelele. Aidha, Ujenzi wa bwawa la maji Maratani unaogharimu bilioni 1.4 unaendelea.
Akizungumzia Huduma za Afya, Ndg. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi katika Ilani yake ya 2020-2025 kitaendelea kuboresha huduma za Afya kwa kuongeza hospitali 98 za Halmashauri nchini, hospitali 10 za Rufaa ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za Bima ya Afya.
Mwaka 2015-2020 wilayani Nanyumbu umefanyika Ujenzi wa Kituo cha Afya Mtambaswala unaogharimu shilingi milioni 400, Ujenzi wa wodi wa wazazi Hospitali ya Mangaka Milioni 400, Ujenzi wa Jengo la mionzi (X-Ray) hospitali ya Wilaya ikiwa ni pamoja na Ujenzi unaoendelea wa Kituo cha Afya Mikangaula unaogharimu milioni 200.
Chama cha Mapinduzi kupitia Mgombea mwenza kimeahidi kuwa ikiwa kitapata ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mitano tena kitaendelea na sera yake ya Elimu bure ili kuhakikisha wanafunzi wanapata haki yao ya kimsingi ya Elimu.
Ifikapo 2023 Tanzania yote itakuwa na umeme, alisema Ndg. Samia Suluhu Hassani akizungumzia Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijiji ambao upo hatua ya tatu (REA III).
Akizungumzia suala la miundombinu ya barabara Mjini Mangaka, Ndg. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa ujenzi wa lami kilomita saba utatekelezwa. Aidha, Wakala wa barabara mijini na vijijini (TARULA) itaendelea kuongezewa bajeti ili kuimarisha miundombinu ya barabara.
Mgombea Ubunge Jimbo la Nanyumbu Ndg. Yahya Ally Mhata pamoja na wagombea udiwani wa Kata za Kilimanihewa na Mangaka kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi wameelezea namna Serikali inayosimamiwa na CCM ilivyotekeleza Miradi mikubwa Nanyumbu ukiwemo mradi mkubwa wa kimkati wa Ujenzi wa Stendi ya Kisasa ya Mabasi Mangaka unaogharimu Shilingi Bilioni 2.1. Aidha, Wagombea hao wameomba wananchi kuwachagua katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 28/10/2020.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.