Meneja wa Bima ya Afya wa Mkoa wa Mtwara Dr. Adolf Kahamba akizungumza na viongozi wa Vyama vya Msingi vya Ushirika
Na, Lunanilo L. Ngela
Akizungumza na viongozi hao Dr. Adolf Kahamba amewaeleza juu ya mpango wa Ushirika Afya ulioanzishwa na mfuko wa wanachama wa vyama vya msingi vya ushirika wa mazao matano ya kimkakati ikiwemo pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku.
Mpango huo unatoa fursa kwa mkulima kujisajili katika mfuko wa Bima ya Afya kupitia chama chake cha msingi cha ushirika. Mkulima atajisajili kwa shilingi 76,800 tuu na kunufaika na huduma ya watu sita kwa mwaka mzima huku wakipata matibabu katika vituo zaidi ya 6,000 vilivyosajiliwa na mfuko nchi nzima. Aidha, mwanachama akitaka kuwasajili watoto chini ya miaka 18 atalipa shilingi 50,400 tuu.
Meneja huyo akizungumzia mafao yatolewayo kwa wanachama wa Bima (NHIF) kupitia mpango wa Ushirika Afya amesema, mafao hayo yanahusisha gharama za kujiandikisha na kumwona daktari, dawa zote mhimu zilizoidhinishwa na Serikali, vipimo vidogo na vikubwa, kulazwa, upasuaji mdogo na mkubwa, matibabu ya kinywa na meno, matibabu ya macho pamoja na miwani ya kusomea, mazoezi ya kimatibabu ya viungo (physiotherapy) na vifaa saidizi kama mangongo na vishikizi vya shingo.
Viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika wametoa shukrani zao kwa Serikali kwa kujumuishwa katika mfuko wa Bima ya Afya kupitia mpango wa Ushirika Afya. Aidha, wameshauri maboresho yafanyike kwa kuandaa utaratibu kupitia teknolojia ya mawasiliano utakaomtaarifu mwanachama juu ya ukomo wa kadi yake ikiwa ni pamoja na kutengenezwa utaratibu rahisi wa kulipia (control number) pindi kadi ikiisha muda ili mwanachama aweze kulipia akiwa sehemu yeyote.
Halmashauri ya Wilaya Nanyumbu
Anwani ya Posta: 246, Masasi
Simu: 0232934112/3
Simu za Mikononi:
Barua Pepe: info@nanyumbudc.go.tz
Copyright ©2017 Nanyumbu Distict Council . All rights reserved.